Back to top

Kilimo cha alizeti kuwa kilimo cha mkataba.

09 June 2021
Share

Serikali imesema kuwa  kuanzia msimu wa kilimo wa 2021/2022 kilimo cha alizeti kitakuwa ni cha mkataba na mpaka sasa Wizara imewasiliana na Waheshimiwa Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji ili kusimamizi Kilimo Mkataba.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Husen Bashe wakati akijibu swali la Mhe.Mussa Ramadhani Sima Mbunge wa Singida Mjini aliyetaka kujuwa Serikali ina mpango gani wa kuimarisha kilimo cha mkataba kwa njia ya Outgrower Scheme ili kupanua wigo wa upatikanaji wa soko kwa wakulima wadogo wadogo.

Mh Bashe akasema kuwa Kilimo cha Mkataba kimeleta matokeo mazuri katika zao la ngano katika mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha. Aidha, makampuni ya Pyxus Agriculture Tanzania Limited, Mount Meru Millers Ltd, Mwenge Sunflower Oil Mills Company Limited na Jackma CO. Ltd yamefanya vizuri katika mikoa ya Manyara, Dodoma na Singida.

Akaongeza kuwa  kilimo cha Mkataba kinawezesha wakulima kuwa na soko la uhakika na wanunuzi kununua mazao yenye ubora kulingana na mahitaji . Aidha, Dhana ya Kilimo cha Mkataba ni kuchangia kutatua changamoto za upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kuimarisha upatikanaji wa mitaji kutokana na makubaliano baina ya mkulima, Taasisi za fedha na wanunuzi wa mazao husika kulingana na mahitaji ya soko.

Aidha Mh Bashe akaongeza kuwa , kwa kutumia Kilimo cha Mkataba Wizara kwa kushirikiana na Sekta binafsi inaendelea kuhamasisha wakulima kushiriki katika kilimo cha Mkataba ambacho kimeonesha mwelekeo mpya katika kuhakikisha masoko ya uhakika, bei nzuri na viwango bora vya mazao ya kilimo.