Back to top

KINA CHA MAJI YA BAHARI YA HINDI CHAONGEZEKA

05 April 2024
Share

Tafiti zimeonesha kuwa kina cha maji ya bahari ya Hindi kimeongezeka kutokana na kuendelea kupanda kwa joto la dunia linalosababisha kuendelea kuyeyuka kwa barafu katika maeneo mbalimbali ya duniani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Selemani Jafo, amesema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini Prof.Patric Ndakidemi aliyetaka kujua kama kweli kina cha bahari ya Hindi kimeongezeka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mhe.Jafo amesema kwa mujibu wa utafiti na vipimo vilivyopo maji ya bahari ya Hindi katika pwani ya Dar es Salaam yanaongezeka kwa wastani wa milimita sita kwa mwaka tangu mwaka 2002.

Amezitaja athari za kuongezeka kwa maji ni pamoja na kuongezeka kwa mmomonyoko na upotevu wa fukwe, mafuriko ya mara kwa mara, uharibifu wa miundombinu kama gati za bandari, barabara, nyumba na masoko, upotevu wa bioanuwai muhimu ikiwemo mikoko na nyasi bahari na upotevu wa ardhi ya kilimo na makazi.