
Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ ), MT 89487 CPL Hamis Ramadhan (36) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam akikabiliwa na shitaka ya kukataa amri halali.
Mshitakiwa huyo amesomewa shitaka na wakili wa serikali Vailet Kyendesya mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Rahim Mushi.
Kyendesya alidai mnamo Februari 7, Mwaka huu mshitakiwa akiwa eneo la Mlimani City barabara ya Survey, Kinondoni, Dar es Salaam akiendesha gari namba T. 433 ALB Nissan Patrol alisimamishwa eneo la kivuko cha watembea kwa miguu na askari Polisi ambapo alikaidi na kuanza kumsukuma askari kwa gari yake.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mshitakiwa alikana makosa yake na kuachiwa kwa dhamana.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 6, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
