
Shirika la Legal Services Facility (LSF) limetoa ruzuku yenye thamani ya shilingi za kitanzania bilioni 3.1 kwa wadau wake nchini, ambao ni mashirika nufaika ya wasaidizi wa kisheria, mashirika simamizi kwenye kanda sita, pamoja na mashirika mengine yanayotekeleza miradi kwenye maeneo muhimu ya kijamii (Thematic areas) hasa uchumi kwa ajili ya uwezeshaji kisheria kwa wananchi ikiwemo wanawake na watoto.
Akiongea kuhusu ruzuku hizo na matokeo yanayotegemea kupatikana, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema "Ruzuku inayotolewa kwa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria inakwenda kuchochea pia utekelezaji mkakati wa kamapeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia uliojikita kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto kwa kutoa elimu katika jamii kuhusu haki za biandamu, kupambana na ukatili wa kijinsia, utatuzi wa migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, kuelimisha wananchi kuhusu mifumo ya sheria, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na kujenga uwezo miongoni mwa wadau wa sekta ya msaada ya kisheria nchini"
Amesema ruzuku yenye thamani ya shilingi bilioni 2.08 imetolewa moja kwa moja kwa mashirika 184 ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar kwenye kila ngazi ya mkoa na wilaya zote kwa ajili kukuza upatikanaji wa haki kwa wananchi kupitia utoaji wa huduma za msaada wa kisheria bure.
Aidha ameongeza kuwa Sehemu ya ruzuku hiyo imetolewa kwa mashirika sita yatakayosimamia mashirika takribani 92 ya wasaidizi wa kisheria katika kanda sita nchini ili kuongeza ubora, uwezo na maendeleo ya kitaasisi katika kutoa huduma bora za msaada wa kisheria kwa mwaka 2023.
