Back to top

Maadhimisho ya Kimondo cha Mbozi kufanyika mwezi Juni mkoani Songwe.

14 May 2018
Share

Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wengine wa uhifadhi na maendeleo utafanya maadhimisho ya siku ya Kimondo cha Mbozi kwa mara ya kwanza katika Kijiji cha Ndolezi Kata ya Mlangali, wilayani Mbozi kuanzia Juni 28 hadi 30 mwaka huu .

Maadhimisho hayo yataenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Vimondo duniani ambayo yaliazimiwa kufanyika Juni 30 kila mwaka na kikao cha Umoja wa Mataifa cha tarehe 6 Desemba, 2016.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho pia kiliazimia tarehe hiyo kuwa siku ya kuelimisha umma kuhusu elimu ya anga na mafanikio yaliyopatikana kuhusu tafiti mbalimbali zilizofanywa kwenye anga za juu, kutambua juhudi zilizofanyika, kuweka sheria za kimataifa na kutoa tahadhari juu ya athari zinazoweza kutokea endapo dunia itafanya uharibifu juu ya anga.

Taarifa hiyo imetolewa jana katika Kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Herman Tesha wakati akiwasilisha taarifa ya maandalizi ya maadhimisho hayo kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga aliyetembelea kimondo hicho kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya maadhimisho hayo.

Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kutangaza Kimondo kama kivutio muhimu cha utalii mkoani Songwe pamoja na vivutio vingine vya mkoa kwa ujumla ili kutoa fursa ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii mkoani humo.

Amesema maadhimisho hayo yataenda sambamba na kongamano la uwekezaji na la sayansi ya vimondo, maonesho ya malikale, maonesho ya kiutamaduni, mashindano ya riadha (Kimondo Marathon), mashindano ya netiboli na mpira wa miguu (Kimondo Ligi).

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema Serikali kupitia Wizara yake itashiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo kwa kushirikiana na mkoa wa Songwe ili kuhakikisha kivutio hicho cha Kimondo kinajulikana zaidi ndani na nje ya nchi na hatimaye kiongeze idadi ya watalii na mapato.

Amesema wizara yake ina mkakati maalum wa kuimarisha kituo hicho cha utalii ambapo hivi sasa imeshajenga kituo maalum cha taarifa ambacho kimegahrimu zaidi ya Shilingi milioni 400 za Kitanzania.

Aidha, amesema kupitia mkakati mpya wa wizara wa kuimarisha na kuvijengea uwezo vituo vya malikale nchini kwa kuzishirikisha taasisi za uhifadhi wa wanyamapori, Hifadhi ya Taifa ya Tanapa itashirikiana na kituo hicho kwa kuimarisha miundombinu na pamoja utangazaji.

Nao wananchi wa kijiji cha Ndolezi wakizungumza kwa nyakati tofauti hawakusita kuonyesha furaha zao kuhusu maendeleo ya eneo hilo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika mipango na miradi mbalimbali itakayoanzishwa katika eneo hilo kwa faida ya pande zote mbili.

Kimondo cha Mbozi kilianguka mwaka 1840 kutoka kwenye obiti yake huko angani na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11. Kimondo hicho ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na cha nane duniani kati ya vimondo 600 vilivyodondoka sehemu mbalimbali, sifa yake kubwa ni kuwa na ubaridi wakati wote hata mchana wa jua kali.