Back to top

MABORESHO BWAWA LA MTERA YAONGEZA UZALISHAJI UMEME

27 November 2025
Share

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, tarehe 26 Novemba 2025, alitembelea na kukagua Kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera kilichopo mpakani mwa mikoa ya Iringa na Dodoma na kuridhishwa na hali ya uzalishaji wa umeme katika kituo hicho muhimu kinachozalisha umeme kwa nguvu ya maji.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhe. Makamba ameeleza kuwa hatua mbalimbali za maboresho yaliyofanyika katika kituo hicho yameongeza ufanisi na uhakika wa upatikanaji wa umeme, hususan katika mikoa ya Iringa na Dodoma.

“Mara baada ya maboresho haya, mitambo hii iko katika hali nzuri na inatuhakikishia uzalishaji wa kutosha. Wananchi wa Dodoma, Iringa na maeneo ya jirani wanaendelea kufurahia umeme wa uhakika,” alisema Mhe. Makamba.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa ulioendelea kufanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika nchini.

“Zaidi ya shilingi bilioni 10 zimetumika kukarabati na kuboresha mitambo miwili ya uzalishaji hapa Mtera. Hayo yasingewezekana bila dhamira ya dhati ya Mhe. Rais kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi,” alieleza.

Aidha, Mhe. Makamba ametoa wito kwa wananchi wote wanaoishi karibu na vyanzo vya maji vinavyozunguka Bwawa la Mtera, ikiwemo Bonde la Ihefu, kuvilinda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Nishati ni uti wa mgongo wa uchumi. Tukiharibu vyanzo vya maji, tunahatarisha uzalishaji wa umeme unaoliwezesha Taifa kusonga mbele,hivyo nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuvitunza vyanzo hivi", alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji Umeme wa TANESCO, Mhandisi Athanasius Nangali, amesema kuwa Kituo cha Mtera kinaendelea kufanya kazi kwa ufanisi wa juu, na kuwa kwa sasa hali ya uzalishaji  ipo vizuri  katika kiwango kinachohitajika.

“Kwa sasa Kituo chetu cha Mtera kina uwezo wa kuzalisha Megawati 80 ambazo ndizo kiwango cha juu cha uwezo wake. Hali hii ya uzalishaji inasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini,” alisema Mhandisi Nangali.

Aliongeza kuwa usimamizi wa miundombinu na vyanzo vya maji vinavyolihudumia Bwawa la Mtera ni jukumu la pamoja kati ya Shirika, Serikali na Wananchi wote kwa ujumla kwani moundombinu ikiwa katika hali ya usalama inachangia upatikanaji wa umeme wa kutosha na kupunguza hali ya kukatika kwa umeme kunakosababishwa na uharibifu wa miundombinu. 

“Kama Shirika tunaendelea kuwasisitiza wananchi kulinda miundombinu ya umeme pamoja na vyanzo vya maji ili kuwezesha TANESCO kuendelea kutoa huduma bora, salama na ya uhakika", aliongeza.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara za Naibu Waziri wa nishati kutembelea na kukagua taasisi zilizo chini ya wizara kwa lengo la kutambua shughuli zao zinavyoendeshwa.