
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, amewataka wananchi kuwa walinzi wa mbolea ya ruzuku iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ya kuongeza uzalishaji wa mazao katika msimu wa 2022/2023.
Amesema kumekuwa na Watanzania wachache wasiokuwa na nia njema wanaotorosha mbolea kwenda nchi jirani na kuwaacha Watanzania, bila kuwa na mbolea ya kutosha.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo, wakati akisalimia na wananchi kwenye eneo la Mbalizi Jijini Mbeya, akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo, inayotekelezwa na Serikali.
Amesema utoaji wa ruzuku hiyo ya mbolea unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na ni marufuku kuiuza nje.
Ameongeza kuwa awali mbolea iliuzwa kwa zaidi ya shilingi 100,000 lakini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia akaridhia kutoa ruzuku shilingi bilioni 150 ili ikashushe bei ya mbolea na sasa inauzwa kwa shilingi 70,000.
