Back to top

MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KWA VYAMA VYA USHIRIKA YALETE TIJA KWA WAKULIMA

28 April 2025
Share

Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Viongozi wanaosimamia Vyama vya ushirika nchini Tanzania kukuza matumizi ya Teknolojia katika uendeshaji wa Vyama hivyo pamoja na kuongeza ubunifu zaidi ili kupanua wigo wa kuhamasisha wakulima kujiunga zaidi na vyama vya ushirika vilivyopo nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza pia umuhimu wa kusimamia ushirika nchini ili kuwa bora zaidi, akisisitiza usimamizi madhubuti wenye kuzingatia misingi ya uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kuleta tija iliyokusudiwa katika kuboresha maisha ya wakulima wa nchini Tanzania.

Akizungumza wakati akizindua Benki ya Taifa ya Ushirika Mjini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Rais Samia akiwahimiza pia Viongozi hao wa vyama vya ushirika nchini kuzungumza na mifuko ya jamii na Taasisi za Bima za afya ili kuweza kuwasaidia Wakulima kupata fursa za uhifadhi na Bima za afya kwaajili ya Matibabu.

Akizungumzia Jitihada mbalimbali ambazo serikali yake imeendelea kuchukua katika kustawisha Vyama vya ushirika nchini, Rais Samia ametoa rai pia ya kuchangamkia masoko mbalimbali yanayotafutwa na serikali ikiwemo soko la Parachichi, mashudu meupe pamoja na soko la Mihogo nchini China ambapo mahitaji ya China ni makubwa kuliko kiwango cha uzalishaji wa mihogo unaofanyika kote nchini Tanzania kwahivi sasa.

Rais Samia pia katika hotuba yake amezungumzia mpango wa serikali yake wa ujenzi wa Viwanda kwa kuhakikisha Vyama hivyo vya ushirika vinakuwa na viwanda katika maeneo yao kwaajili ya kuongeza thamani ya mazao yao kuendana na soko linavyohitaji, akisisitiza umuhimu wa kujenga imani kwa wananchi kwa kuwasomea ripoti za mapato na matumizi kulingana na taratibu ,a uendeshaji wa Vyama hivyo nchini.