Back to top

MIKAKATI YA UINGEREZA KWENYE SEKTA YA AFYA

06 April 2024
Share

Serikali ya Uingereza imetangaza mipango na mikakati mipya ya ushirikiano na Serikali ya Tanzania, ili kuimarisha ushirikiano katika Sekta za Afya, Uwekezaji na Biashara na kusaidia miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Mipango hiyo imetangazwa Jijini Dodoma na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika, Mhe.Andrew Mitchell, wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi Ndogo za Ubalozi wa Uingereza humo.

Mhe. Mitchell amesema Serikali ya Uingereza imechangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 18.9 kwenye Mpango wa Miaka Mitano wa Afya kwa Wote unaotekelezwa nchini ili kuimarisha mifumo ya afya, kuimarisha ustahimilivu wa huduma za afya, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Kadhalika, Uingereza imetoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 15 kwa ajili ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwenye masuala ya maboresho ya  Afya ya Uzazi ikiwemo kuboresha huduma za uzazi wa mpango kwa lengo la kuwafikia takribani watu 900,000.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.January Makamba, ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kwa kutangaza mipango na ufadhili kwa miradi mbalimbali ya manufaa kwa wananchi wa Tanzania.

Pia ameipongeza nchi hiyo kwa kufungua Ofisi Ndogo za Ubalozi Jijini Dodoma, ikiwa ni mwitikio wa wito wa Serikali ya Tanzania wa kuhamishia Makao Makuu yake Jijini humo.