
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imethibitisha taarifa za kifo cha Bw. Clemence Felix Mtenga, Kijana Mtanzania ambaye ni miongoni mwa Watanzania wawili, ambao pamoja na raia wa mataifa mengine walikuwa hawajulikani walipo tangu yaliyopotokea mapigano tarehe 07 Oktoba, 2023, nchini Israel na katika maeneo ya Wapalestina hususani Gaza.
Marehemu Clemence alikuwa ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wapatao 260 waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya Mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.
Wizara imesema tayari imechukua hatua stahiki ikiwemo kuijulisha familia na inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Israel kuhakikisha kwamba taratibu za kuurejesha mwili wa Marehemu nchini kwa ajili ya mazishi zinakamilika kwa wakati.
Aidha, Wizara imesema inaendelea kufuatilia taarifa za Mtanzania mwingine Ndugu Joshua Mollel ambaye bado hajulikani alipo tangu yalipotokea mashambulizi hayo.