Back to top

MTWARA: NYUMBA ZAIDI YA 800 KUUNGANISHIWA GESI YA KUPIKIA

13 May 2025
Share

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inatarajia kuunganisha mfumo wa gesi ya kupikia katika nyumba takribani 865 mkoani Mtwara kwenye maeneo ambayo yana miundombinu ya bomba la gesi.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 13, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Tunza Malipo aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kuunganisha gesi kwa Taasisi na Nyumba za Wananchi mkoani Mtwara kwa ajili ya kupikia.
 
"Katika Mkoa wa Mtwara, Serikali imeshapeleka miundombinu ya usambazaji gesi asilia katika baadhi ya maeneo ambapo jumla ya nyumba 425 na Taasisi nne (4) zimeunganishwa na mtandao wa matumizi ya gesi asilia katika maeneo ya Mtwara mjini."  Amesema  Kapinga

Ameongeza kuwa,  katika nyumba hizo 865 zitakazounganishwa na mfumo,  Serikali imeshafanya usanifu wa kihandisi kwa ajili ya kwenda hatua ya kuunganisha.

Ameweka bayana kuwa,  tayari Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Dkt. Doto Biteko ameshauagiza  Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na TPDC  kushirikiana ili  kuongeza kasi ya kuunganisha gesi asilia kwa wananchi wa Mtwara na Lindi. 

Akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Mhe. Dorothy Kilave aliyeuliza kuhusu Serikali kuona umuhimu wa kuharakisha kuunganisha gesi kwenye masoko kama vile Sterio, Temeke, Keko na Mtoni kwa ajili ya Mama Lishe na Baba Lishe, Mhe. Kapinga amesema  Serikali inao mkakati kupitia TPDC kuunganisha gesi asilia katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. 

Ameeleza kuwa, kwa masoko ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja Serikali imeyachukua na itaenda kuyafanyia tathmini.

 Mbunge wa Momba, Mhe. Mhe. Kondesta Sichwale kwa upande wake aliuliza kuhusu suala la  mitungi ya ruzuku kufikia idadi ndogo ya wananchi na kuishauri Serikali kupeleka mitungi ya ruzuku kwa watendaji wa Kata ili kila mwananchi achukukulie hapo kwa kitambulisho cha NIDA.

 Kuhusu suala hilo Kapinga amesema Serikali inaanza kugawa mitungi ya ruzuku takribani  420,000 ambapo utaratibu ni kila mwananchi kuchukua mtungi wa gesi kwa kutumia namba yake ya NIDA ama kitambulisho cha NIDA  ili kumuwezesha mwananchi mmoja kupata mtungi mmoja.

Ameongeza kuwa,  Serikali pia ilitenga mitungi  3,255 kwa kila Wilaya ikiwa ni hatua ya kuanza kwa mkakati wa nishati safi ya kupikia ambapo amewahakikishia Wabunge kuwa mkakati huo ni wa miaka kumi na endelevu.

Mhe. Kapinga ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka kumi asilimia 80 ya watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia ambayo ndio maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.