
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kwenye kilimo na akawataka wenye mitaji waje kuwekeza Tanzania ambapo wataweza kufikia soko la watu milioni 170 kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akieleza fursa zilizopo, alitaja usindikaji na ufungashaji wa mazao, maghala, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa katika ubaridi, usafirishaji, huduma za kidijitali na huduma za kifedha kwa wakulima na wafanyabiashara.
Ameyasema hayo wakati akiongoza mjadala kuhusu uwekezaji kwenye kilimo biashara uliowahusisha viongozi wa kampuni za utafiti wa kilimo na teknolojia za kilimo, uzalishaji bidhaa za kilimo, mbegu na dawa za wadudu wa mazao yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), jijini Des Moines, Jimbo la Iowa, Marekani.
Akifafanua, Dkt. Mwigulu alisema Tanzania ina hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo, lakini zinazotumika ni hekta milioni 10.8 pekee. Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, alisema nchi ina uwezo wa kumwagilia hekta milioni 29.4, lakini kwa sasa zinazotumika ni hekta 727,28 hali inayotoa fursa kubwa kwa wawekezaji.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali imewekeza katika skimu za umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu na programu za kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo, mifugo na uvuvi. Vilevile, imeweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa sekta binafsi ni mshirika muhimu katika kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko, kutengeneza ajira zenye staha na kuimarisha usalama wa chakula na lishe.
Akichangia mjadala huo kuhusu matumizi ya Akili Unde (AI) katika kilimo, Mkurugenzi Mtendaji wa Utafiti na Viwanda wa Kampuni ya Microsoft, Dkt. Ranveer Chandra alisema alianzisha programu ya kilimo ndani ya Microsoft miaka 10 iliyopita na tangu wakati huo, wametekeleza shughuli mbalimbali nchini Tanzania.
Kuhusu kuongeza ujuzi wa akili unde, Dkt. Ranveer Chandra alisema wameshirikiana na ABSA Tanzania pamoja na Women in Tech kutekeleza mpango unaolenga kuwapatia wanawake 5,000 mafunzo kuhusu akili unde.
Amesema akili unde haipaswi kuchukuliwa kama mbadala wa mkulima, bali kama nyenzo ya kuongeza maarifa na uwezo wa mkulima kufanya maamuzi sahihi.
Amesema Tanzania ina faida zaidi kutokana na nafasi yake ya kimkakati kama lango la kuunganisha masoko ya kikanda.

