Back to top

WAFANYABIASHARA 10 WAFARIKI BAADA YA LORI KUTUMBUKIA MTONI UGANDA

26 November 2026
Share

Takriban watu 10 wamepoteza maisha baada ya lori lililokuwa likibeba abiria kuanguka na kutumbukia mtoni katika wilaya ya Zombo, kaskazini-magharibi mwa Uganda. Polisi wamesema watu wengine wanne wamejeruhiwa vibaya katika ajali hiyo.

Waliofariki walikuwa wafanyabiashara waliokuwa wakirejea nyumbani kutoka soko la kila wiki wakati ajali ilipotokea.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi wa Uganda, lori hilo lilikuwa limebeba mifugo na liliondoka katika Soko la Loro lililoko wilayani Lira siku ya Jumatano kabla ya kufika mji wa Zombo majira ya saa 1:00 usiku. Asubuhi iliyofuata, lori hilo lilipakiwa magunia ya unga wa muhogo pamoja na abiria kwa safari ya kurejea Lira.

Wilaya ya Zombo, inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), iko takribani kilomita 410 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Uganda, Kampala.

Mamlaka zimesema operesheni za uokoaji na kurejesha miili zinaendelea, huku kukiwa na hofu kwamba huenda watu wengine bado wamenaswa chini ya maji.

Ajali za barabarani zimeendelea kuwa changamoto kubwa nchini Uganda. Kwa mujibu wa Ripoti ya Uhalifu ya Polisi wa Uganda ya mwaka 2025, nchi hiyo ilirekodi ajali za barabarani 26,044 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.7 ikilinganishwa na ajali 25,107 zilizorekodiwa mwaka 2024.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani viliongezeka hadi 5,383 mwaka 2025, kutoka 5,142 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 4.7.

Sababu kuu ya ajali hizo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni kupita magari mengine bila tahadhari (careless overtaking), jambo lililochangia asilimia 21.8 ya ajali zote zilizorekodiwa nchini humo.