Back to top

WAFUGAJI WAPATIWA ELIMU KUDHIBITI MAGONJWA YA MIFUGO MOROGORO

27 November 2026
Share

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imetoa elimu kwa vitendo kuhusu huduma inazozitoa kwa wadau wa mifugo, zikiwemo uzalishaji wa chanjo za mifugo, uchunguzi wa magonjwa na uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, Elimu hiyo imetolewa kwa wadau waliotembelea banda lake katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro.

Utoaji wa elimu hiyo umeongozwa na Dkt. Jumanne Jumbe, akiwa pamoja na Dkt. Scholastica P. Doto na Bw. Paulo Joseph, kwa kutumia vifaa, sampuli na vielelezo mbalimbali wakati wa maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya tiba ya wanyama nchini Tanzania. Maonesho hayo yameanza Novemba 24 na yanatarajiwa kumalizika Novemba 27, 2026, huku miongoni mwa waliotembelea banda la TVLA na kupatiwa elimu wakiwa wahadhiri, wanafunzi na wafugaji.

Kuhusiana na chanjo za mifugo, TVLA imeonesha aina saba za chanjo zilizopo sokoni na kufafanua shughuli za uzalishaji na upatikanaji wake.
Kwa upande wa huduma za maabara, Wakala imeonesha kwa njia ya picha vifaa vya kisasa ambavyo havikuweza kusafirishwa, pamoja na vifaa vilivyokuwapo kwenye maonesho, vikiwemo vifaa vya ELISA, PCR na hadubini. Wataalamu wamefafanua matumizi yake katika uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama, pamoja na uchunguzi wa sampuli mbalimbali kitu kilichowavutia baadhi ya wahadhiri wa SUA, ambao wameambatana na wanafunzi ili wajifunze kuhusu huduma hizo na kujionea vifaa vinavyotumika.

Sambamba na hilo, wataalamu wametoa elimu kuhusu uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo na namna TVLA inavyotekeleza jukumu hilo. Sampuli za vyakula vya mifugo zilizowekwa bandani zimetumika kufafanua huduma za upimaji na uhakiki wa ubora zinazotolewa na Wakala.

Kuhusiana na tatizo la kutupa mimba kwa mifugo, TVLA imetumia vielelezo vya ndama vilivyohifadhiwa kwenye chupa kutoa elimu kwa wageni. Kupitia vielelezo hivyo na maelezo ya wataalamu, wageni wamepatiwa elimu kuhusu brucellosis na udhibiti wake. Aidha, wameelimishwa kuhusu kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya dawa za mifugo na kuzingatia ubora wa chakula cha wanyama.

TVLA pia imetoa elimu kuhusu uhakiki wa ubora na usajili wa viuatilifu vya mifugo. Sambamba na hilo, wageni wameoneshwa aina mbalimbali za mbung’o na kupatiwa elimu kuhusu namna ya kuwadhibiti.