Back to top

MWIGULU ASHAURI KUFANYIKA UTAFITI WA VIKWAZO VYA KUFIKIA MALENGO.

12 May 2023
Share

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezishauri nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya utafiti ili kufahamu sababu za nchi hizo kushindwa kufikia vigezo mtangamano wa uchumi mpana ambavyo ni moja kati ya vigezo vya nchi hizo kufanikisha itifaki ya Umoja wa Sarafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2031.

Dkt. Nchemba alitoa rai hiyo, wakati wa mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha, na Uchumi la Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika Jijini Arusha, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulipokea na kujadili taarifa mbalimbali za mkutano uliopita wa Baraza hilo.

Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na mashauriano ya kibajeti,  kwa mwaka wa fedha 2023/2024, taarifa ya Mkutano wa 26 wa Kamati ya Magavana wa Benki Kuu za Jumuiya hiyo; Mwenendo wa hali ya uchumi na maendeleo ulimwenguni pamoja na hatua zilizofikiwa na nchi wanachama katika kukidhi vigezo vya mtangamano wa uchumi mpana wa Jumuiya hiyo. 

Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania imekidhi vigezo vyote vya mtangamano wa uchumi mpana isipokuwa kigezo cha nakisi ya bajeti kinachopaswa kuwa chini ya asilimia 3. Kwa upanda wa Tanzania kigezo hicho kimefikiwa kwa asilimia 3.3 wakati nchi zote za Jumuiya hiyo zikishindwa pia kufikia kiwango kinachotakiwa ili kuwezesha kufikiwa kwa Umoja wa Fedha unaolenga kuwa na sarafu moja.