
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Emmanuel Nchimbi amemuelekeza Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhakikisha utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa - Omurushaka Karagwe (km 62.5) kwa kiwango cha lami unaanza mara moja, ili kuondoa adha wanazozipata wananchi wa Wilaya ya Kyerwa na Karagwe.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa Kyerwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Stendi ya Mabasi ya Nkwenda, Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuahidi Katibu Mkuu Dkt. Nchimbi kumleta na kumkabidhi kwa wananchi Mkandarasi aliyepatikana kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa - Omurushaka (km 62.5) kwa kiwango cha lami na tayari Mkandarasi ameshaoneshwa eneo la kujenga Kambi na eneo la kuweka mitambo ili kuanza ujenzi wa barabara hiyo.
