Back to top

NDUMBARO, ELIAKIM MASWI WATUNUKIWA TUZO YA SHUKRANI

28 April 2025
Share

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga, amewatunuku tuzo ya Shukrani Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Eliakim Maswi kwa kutambua na kuthamini juhudi na mchango wao katika kuhakikisha Watanzania wote wanathaminiwa na kupata Haki zao. 

Mhe. Nderiananga amesema kuwa, kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia watoto, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu wamefanikiwa kupata Haki zao baada ya kutatuliwa changamoto zao mbalimbali zilizokua zinawakabili.

Wakizungumza kwa wakati tofauti Waziri  Ndumbaro amemshukuru Mhe. Nderiananga kwa kumpatia tuzo hiyo ambapo amekiri kuwa itamuongezea ari ya utendaji katika kuwatumikia Watanzania na kuhakikisha Haki ya kila mwananchi mnyonge inapatikana.

Naye Katibu Mkuu Bw. Eliakim Maswi amesema kuwa, tuzo hiyo ni ishara ambayo itaendelea kumkumbusha kutimiza  wajibu wake wa kuwatumikia Watanzania kwa ufanisi  ili kuwaletea maendeleo.

Ikumbukwe kuwa Wizara imeendelea kutekeleza  Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambapo mpaka sasa jumla ya mikoa 25 ya Tanzania Bara imefikiwa na kwa sasa utoaji wa Huduma unaendelea katika Mkoa wa Kaskazini Unguja Zanzibar.