Back to top

NYANDA ZA JUU KUSINI ENEO LA KIMKAKATI KWA UFUGAJI NG'OMBE WA MAZIWA.

25 March 2024
Share

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi, amesema Wizara yake imeifanya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kuwa ni eneo lao la kimkakati kwa upande wa Ufugaji hususani ufugaji wa Ng’ombe wa Maziwa.

Prof. Mushi amebainisha hayo, wakati akifungua mafunzo rejea kwa maafisa ugani wa mikoa iliyopo kwenye kanda hiyo, tukio lililofanyika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe ambapo amesema licha ya Kanda hiyo kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula kwa ujumla, Wizara yake inaitambua kama kinara wa ufugaji wa ng’ombe bora wa maziwa.

Prof. Mushi amesema kuwa ushiriki wa maafisa Ugani kwenye mafunzo hayo utaisaidia Wizara kutafsiri kwa vitendo mipango na mikakati ya Wizara yake katika kuboresha sekta ya Mifugo nchini na kuishusha tafsiri hiyo kwa wafugaji ili waweze kuitekeleza.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Songwe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi mbali na kuipongeza Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo amewataka Maafisa Ugani hao kutumia mafunzo hayo kama sehemu ya nyenzo za kwenda kuwafundishia wafugaji ili waweze kufuga kisasa na kwa tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa ambao ndio waandaaji wa Mafunzo hayo amesema kuwa jukumu kubwa la Wizara yake ni kuhakikisha maarifa mapya yanawafikia wafugaji wakati wote  kupitia kwa maafisa ugani wao huku wakijikita kwenye kuhakikisha wanaongeza elimu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa upande wa sekta ya Mifugo.  

Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Ugani wenzake, Afisa Ushauri wa Mifugo kutoka Manispaa ya Songea Bw. Edwin Ndunguru ameahidi kwenda kutekeleza kwa vitendo  yote waliyoelekezwa huku pia akitoa rai kwa Serikali kuwaandalia mafunzo ya aina hiyo mara kwa mara.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiendesha Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wote nchini lengo likiwa ni kuhakikisha  wafugaji waliopo nchini wanapewa elimu ya mabadiliko ya tekonolojia yanayotokea mara kwa mara ili waendelee kufuga kwa tija.