Back to top

Rais Samia afanya uteuzi wa Mkuu wa Itifaki (CP) na Mkurugenzi wa eGA

18 April 2021
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemteua Bw. Yusuf Tindi Mndolwa kuwa Balozi.

Pamoja na uteuzi huo, Mhe. Rais Samia amemteua Balozi Mteule Mndolwa kuwa Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocol) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kufuatia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu Aprili 17, imeeleza kuwa Balozi Mteule Mndolwa anachukua nafasi iliyoachwa na Mhe. Balozi Brig. Jen. Wilbert Augustine Ibuge ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Mteule Mndolwa ataapishwa Jumatatu tarehe 19 Aprili, 2021 Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amemteua Bw. Benedict Benny Ndomba kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Kabla ya uteuzi huo, Bw. Ndomba alikuwa Mkurugenzi wa Miundombinu na Operesheni wa eGA na anachukua nafasi ya Dkt. Jabir Bakari Kuwe ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo tarehe 17 Aprili, 2021.