
Rais wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan ameagiza taasisi zote za udhibiti serikalini, kuharakisha maboresho ya sheria, kanuni na taratibu kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji kwa sekta binafsi nchini.
Ameeleza hayo wakati akifungua mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara mkoani Dar es Salaam, Dkt.Samia amekiri mifumo haisomani ndani ya sekta ya umma na kuagiza sekta husika kuharakisha maboresho ili isomane kwa viwango vya kimataifa.
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuongeza uwekezaji katika uboreshaji wa Miundombinu, Nishati na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kuendesha uchumi wa Kidijitali, ambapo ametoa fursa kwa sekta binafsi kuchangamkia uwekezaji katika viwanda vya kuunda simu janja nchini.
Rais Dkt.Samia ameitaka sekta binafsi kuchangamkia fursa ya ongezeko la utalii, kwa kujenga hoteli za kupokea ugeni mkubwa unaotarajiwa nchini kwa miaka inayokuja , kutokana na maboresho ya utangazaji wa vivutio vilivyopo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Bi.Angelina Mgalula ameomba serikali kufanya marejeo ya mfumo wa kodi na tozo ili kwenda na wakati na kuondoa malalamiko.
