Back to top

RAIS SAMIA KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI.

19 March 2023
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanawake kupaza sauti kwa pamoja na kukemea changamoto zinazowakabili wanawake wa Tanzania katika nyanja mbalimbali bila kujali itikadi zao.

Rais Samia ametoa wito huo leo wakati akihutubia katika sherehe ya kilele cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, iliyofanyika katika uwanja wa
Uhuru.

Aidha, Rais Samia ameahidi kuendelea kutafuta suluhu za changamoto zinazowakabili wanawake na kuwafanya kukosa huduma ikiwemo kujenga shule za wasichana za sayansi na vyuo vya ufundi ili kuwainua wanawake katika masuala ya kiteknolojia.

Kwa upande wa miundombinu, Rais Samia amesema Serikali imeweka bajeti ya kutosha kuiwezesha Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuendeleza miundombinu ya barabara vijijini.

Vile vile, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kuimarisha Bandari za Dar es Salaam, Zanzibar, Tanga, Mtwara na Kigoma ili kuimarisha biashara nchini na ndani ya bara la Afrika kwa ujumla.

Halikadhalika, Rais Samia amesema Serikali itasimamia Tanzania kuwa kinara wa uchumi kwa kumsimamia mwanamke kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazouzwa ndani na nje ya nchi kama ilivyopendekezwa na Jukwaa la Usawa wa Kijinsia.

Rais Samia pia ameeleza kuwa changamoto za mabadiliko ya tabia nchi zimesababisha kupanda kwa gharama za bidhaa hivyo, Serikali itaendelea kukabiliana na changamoto hizo kuhakikisha Watanzania wanakuwa na ustawi mzuri wa maisha.