Back to top

REA YAANZA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA NAIBU WAZIRI MKUU DKT. BITEKO

17 November 2023
Share

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeanza utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt. Doto Biteko, wa kuwafikishia huduma ya umeme wakazi wa Madimba na Msimbati kwa kufanya tathmini katika maeneo hayo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, amefanya ziara katika Kata za Madimba na Msimbati ili kuona hali halisi kabla ya kuanza utekelezaji.

Naibu Waziri Mkuu, Dkt Doto Biteko, akiwa katika ziara ya kika zi mkoani Mtwara, hivi karibuni aliitaka REA kuangalia ni namna gani inaweza kuwaunganishia umeme wananchi wa maeneo hayo na kujenga miundombinu ili waweze kunufaika na nishati ya gesi asilia inayozalishwa katika eneo hilo.

Akizungumza na Madiwani wa Kata za Msimbati na Madimba, Balozi Meja Jenerali Kingu, amesema REA itahakikisha maelekezo hayo yanatekelezwa ambapo Novemba 18, 2023 watakutana na mkandarasi kwa ajili ya kujadili ujenzi wa miundombinu ya umeme katika kata hizo.

Aidha, amesema Bodi na Menejimenti ya REA watafuatilia kwa karibu utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri Mkuu la kuyafikishia maeneo hayo umeme.

Ametaka taarifa zitolewe haraka endapo kutakuwa na changamoto katika utekelezaji wa mradi huo ili zipatiwe ufumbuzi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Vijijini, Mhandisi Jones Olotu, amewahakikishia Maafisa Watendaji wa Kata hizo mbili kuwa wiki ijayo wakandarasi watafika kukutana nao kwa ajili ya kuoneshwa maeneo na vijiji vinavyotakiwa kufikishiwa umeme.

Diwani wa Kata ya Msimbati, Rashid Linkon, ameishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kuhakikisha wanapata umeme na kunufaika na rasilimali ya gesi asilia inayopatikana eneo hilo.

Amesema upatikanaji huo wa umeme utaleta hamasa kwa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya uzalishaji wa gesi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Madimba, Idrisa Kujebweja, alitoa pongezi kwa mwitikio wa haraka ambao umeoneshwa na REA katika kufanyia kazi maelekezo ya Naibu Waziri Mkuu na kuahidi kwamba, watatoa ushirikiano wote utakaohitajika.