Back to top

WIZARA YA AFYA YAKAGUA UTAYARI MBEYA DC DHIDI YA EBOLA

30 October 2026
Share

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dkt. Erasto, amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imepokea timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa ajili ya kutathmini maandalizi na utayari wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, hususan ugonjwa wa Ebola, endapo utatokea nchini.

Akizungumza hayo Oktoba 29, 2026 Jijini Mbeya, Dkt.Erasto amesema ziara hiyo ni muhimu kwa kuzingatia jiografia ya Wilaya ya Mbeya, ambayo inapakana na maeneo ya nchi jirani na hutumika kama njia ya kupita kwa magari mengi yanayosafiri kwenda na kutoka nchi hizo. Hali hiyo inahitaji kuimarishwa kwa maandalizi ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko ili kulinda afya za wananchi na kuzuia uwezekano wa maambukizi kusambaa.

Ameeleza kuwa katika ziara hiyo, timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya inafanya tathmini ya Hospitali ya Wilaya ya Mbeya iliyopo Inyala, kwa kuangalia maandalizi yaliyopo, upatikanaji wa vifaa muhimu pamoja na uwezo wa watumishi wa afya katika kukabiliana na wagonjwa au watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi ya Ebola.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbeya, Dkt. Bwire Mbango, amesema kuwa wamefurahi kupokea wataalamu hao ambao wamefika kufanya tathmini ya utayari wa hospitali katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko. Amesema tathmini hiyo inalenga kubaini namna hospitali ilivyojiandaa kumpokea na kumhudumia mgonjwa au mtu anayeshukiwa kuwa na dalili za Ebola kwa kuzingatia taratibu za kinga na udhibiti wa maambukizi.

Dkt. Bwire Mbango ameongeza kuwa baada ya wataalamu hao kukagua maeneo yaliyotengwa na kuandaliwa kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko, wametoa ushauri wa kitaalamu na mapendekezo ya namna ya kuboresha maandalizi yaliyopo. Mapendekezo hayo yanatarajiwa kusaidia kuimarisha utayari wa hospitali, ikiwemo kuboresha mazingira ya huduma na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.

Amesisitiza kuwa maoni na mapendekezo yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ili kuimarisha kinga na udhibiti wa maambukizi, kulinda watumishi wa afya wanapotoa huduma na kuhakikisha usalama wa wagonjwa.