Back to top

BILIONI 25 KUOKOA WATOTO WENYE MARADHI YA MOYO

29 October 2026
Share

Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya afya ambapo watoto kati ya 16,000 hadi 24,000 huzaliwa na matatizo ya moyo kila mwaka, huku takribani 4,000 miongoni mwao wakihitaji upasuaji wa haraka ndani ya mwaka mmoja.

Ingawa Serikali inagharamia asilimia 70% ya matibabu hayo na nchi ikiwa na wataalamu, familia nyingi zimekuwa zikitatizika kumudu asilimia 30 inayobaki kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, jambo linalochelewesha matibabu ya kuokoa maisha ya watoto hao.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ikishirikiana na Heart Team Africa Foundation (HTAF) zimeanzisha mpango wa kukusanya shilingi bilioni 25. 

Mkakati huo unalenga kusaidia gharama za matibabu ya watoto 1,000 wenye matatizo ya moyo katika kipindi cha miaka 4 hadi 5 ijayo, pamoja na kugharimia ujenzi wa 'Nyumba ya Matumaini' itakayotumiwa na watoto wanaotibiwa pamoja na familia zao.

Ili kufanikisha azma hiyo, harambee kubwa ya changizo inatarajiwa kufanyika kupitia hafla ya JKCI–HTAF Prestige Gala Dinner 2026 itakayofanyika Disemba 4, 2026 katika Hoteli ya Malaika Beach jijini Mwanza. 

Hafla hiyo, yenye kaulimbiu "Okoa Moyo wa Mtoto, Okoa Taifa," inatarajiwa kupambwa na Mgeni Rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.