
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel amesema hakuna Wilaya itayokosa gari la kubebea wagonjwa baada ya ununuzi wa magari 727 ya kubebea wagonjwa na magari 146 kwa shughuli za kiutawala, ambapo amebainisha kuwa tayari magari 20 yamepokelewa na magari 117 yapo njiani kutoka kwa mtengenezaji.
.
Dkt.Mollel ameyasema hayo leo Aprili 5, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Ruvuma Mhe. Mariam Madalu Nyoka katika Mkutano wa 11 kikao cha pili, Bungeni Jijini Dodoma ambapo magari hayo yataondoa kero za wananchi wenye uhitaji wa huduma za rufaa kutoka kituo kimoja kwenda kingine.
.
Magari yote yanatarajiwa kuwasili nchini na kukabidhiwa kwenye vituo vya kutolea huduma kabla ya mwezi Juni 2023, na Wizara ya afya itashirikiana na Wizara ya TAMISEMI ili kufikia maeneo yote yenye uhitaji zaidi kulingana na mazingira.
.
Aidha, Dkt. Mollel amesema hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa hospitali zitazonufaika na magari hayo kutokana na uhitaji mkubwa katika Mkoa huo kwenye vituo vya kutolea huduma kuanzia ngazi ya zahanati mpaka Mkoa.
