Back to top

SERIKALI KUBORESHA VITUO VYA FORODHA NCHINI

28 September 2023
Share

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, amesema serikali itaboresha vituo vya Forodha mkoani Kilimanjaro, kwa kuweka vifaa vya kisasa, kuboresha majengo ya ofisi hasa jengo upande wa mizigo (Cargo), kuboresha mazingira ya nyumba za watumishi wa kituo hicho na kuongeza vitendea kazi kama vile mdaki, (Scanner kwa upande wa wageni wanaowasili.

Chande ameeleza hayo alipofanya ukaguzi kwenye kituo cha forodha kilichopo katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).

Mhe. Chande amesema kuwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2023/24, Serikali itahakikisha inaweka kipaumbele kuwapatia Mdaki (Scanner) moja katika kituo hicho cha Forodha cha KIA ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapayo ya Serikali. 

"Katika ziara hii nimetembezwa kuona sehemu zenye changamoto na naahidi kuwa Serikali itafanyia kazi hasa katika kupata mdaki (Scanner) mpya, na vituo vyote vya forodha nilivyotembelea tumeona hii changamoto na Serikali itahakikisha inalitatua"Amesema Mhe. Chande

Ameongeza kuwa, kazi ya Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhee. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika filamu ya Royal Tour, imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya watalii ambapo kupitia Uwanja wa Ndege wa KIA, inategemea kupata zaidi ya watalii milioni moja kwa mwaka sawa na zaidi ya asilimia 80 kwa mara ya kwanza.

"Haitakuwa vyema wageni wa idadi hii wakute changamoto ya foleni kwa sababu ya changamoto ya mdaki, tutaliweka sawa kwa haraka ili wakitoka hapa wawe mabalozi wazuri kuhusu huduma tunazozitoa"Ameongeza Mhe. Chande.

Aidha Mhe.Chande amewaomba watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazi kwa uadilifu ili kukuza ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha huduma wanazotoa kwa walipa kodi iwe ya wazi na kwa uzalendo.

Pia amewaahidi kuboresha mazingira yao ya kazi kwa kuboresha makazi yao yaliyopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ile wakaze katika mazingira yanayokidhi utoaji wa huduma bora kwa wateja.