
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesema Serikali itaweka mifumo ya ufuatiliaji na uwajibikaji katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha mpango huo unawafikia wananchi wa maeneo yote nchini.
Akizungumza Oktoba 22, 2026, wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Usajili wa Bima ya Afya kwa Wote katika viwanja vya Sabasaba mkoani Mtwara, Mchengerwa amesema Serikali itahakikisha utekelezaji wa mpango huo unafuatiliwa kwa karibu kuanzia ngazi ya wilaya hadi ngazi ya taifa.
Amesema katika utaratibu huo, Mabalozi wa Bima ya Afya katika kila wilaya watakuwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha wananchi kujiunga na bima, huku tathmini ya utekelezaji ikifanyika kila mwezi chini ya usimamizi wa Wakuu wa Wilaya na taarifa kuwasilishwa Wizara ya Afya kila robo mwaka.
Ameongeza kuwa utaratibu huo unalenga kutambua changamoto zinazokwamisha uandikishaji wa wananchi, kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati na kuhakikisha juhudi za Serikali zinafikia makundi yote, wakiwamo wananchi wa vijijini na maeneo yenye changamoto za upatikanaji wa huduma.
Mchengerwa amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha hakuna kaya inayoachwa nyuma katika mpango huo, akieleza dhamira ya kuifikia kila kaya, hata ile iliyoko mwisho wa barabara ya mwisho, ili kila Mtanzania awe na nafasi ya kupata huduma za afya kupitia bima.
Ametoa wito kwa viongozi wa mikoa na wilaya, watoa huduma za afya, Mabalozi wa Bima ya Afya na wananchi kushirikiana katika kufanikisha utekelezaji huo, akihimiza mshikamano katika kutimiza kaulimbiu ya kampeni hiyo ya "Bima ya Afya kwa Wote, Uhakika wa Matibabu"
