Back to top

SERIKALI KUONGEZA VITUO 4, HUDUMA ZA MIONZI

05 April 2024
Share

Serikali imesema inaendelea na taratibu za kuongeza vituo vingine vinne vitakavyotumika kutibu wagonjwa wa Saratani kwa njia ya mionzi.
.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu, Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Tunza Issa Malapo, aliyeuliza "Je ni Hospitali ngapi zinatoa huduma ya tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa Saratani hapa nchini?".
.
Mhe.Ummy amesema vituo vitakavyoongezwa ni Hospitali ya Benjamin Mkapa, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Hospitali binafsi ya Aghakhan pamoja na kimoja kwa Visiwani Zanzibar (Hospitali ya Binguni), ambavyo vitajengewa majengo na kuwezeshwa vifaa vitakavyotumika kutibu wagonjwa wa Saratani kwa njia ya mionzi.
.
Aidha, Mhe.Ummy amewataka Waganga Wafawidhi wa vituo vyote vya Serikali vya kutoa huduma za afya hapa nchini, kutenga angalau siku moja kwa kila mwezi, ya watu kupima saratani na madaktari wa Mikoa na Wilaya wasimamie maelekezo hayo ya Serikali na kwamba serikali itaendelea kutumia njia mbalimbali kutoa elimu ili wananchi wajitokeze kupima Saratani kwa kuwa takwimu zinaonesha kila mwaka Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani Elfu 40 na wanaofika kwa ajili ya kupata huduma ni 30%.