Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa amesema serikali ipo katika hatua za mwisho za kuandaa sheria inayosimamia ujenzi wa majengo hasa katika miji na majiji kutokana na mapungufu yaliyopo katika sheria iliyopo sasa ambayo imeleta changamoto ya ujenzi holela katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza Mkoani Dodoma wakati akifungua mkutano wa bodi ya wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi nchini AQRB kwa niaba ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema ni dhamira ya serikali kukamilisha sheria hiyo na kudai kuwa ujio wa sheria hiyo itawezesha katika kupanga mipango miji katika miji na majiji nchini.
Naye waziri wa ujenzi uchukuzi na mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi kuangalia upya viwango vya ada wanavyotoza ili kupanua wigo wa utoaji huduma kwa wananchi.
Awali akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa bodi ya usajili na wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi Dkt. Ludigija Bulamile amesema bodi hiyo inaendelea kuchukua hatua ikiwemo kuwafutia leseni baadhi ya wataalamu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.