Back to top

SERIKALI YA QATAR YATOA MSAADA WA VYAKULA, HANANG

19 February 2024
Share

Serikali ya Qatar imetoa msaada wa vyakula kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope wilayani Hanang mkoani Manyara, ambapo miongoni mwa misaada hiyo ni chakula kikavu katika vifungashio 1440, chakula kilicho tayari kuliwa katika vifungashio 3024 na vifaa vya usafi wa wanawake 4200.
.
Msaada huo umepokelewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga, katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambapo ameishukuru Serikali ya Qatar kwa msaada huo, huku akibainisha kuwa wanatambua michango yote ya wadau wakiwemo wananchi, sekta binafsi, asasi za kiraia na kidini, mashirika ya kimataifa na Umoja wa mataifa.

Picha ya pamoja ya baadhi ya viongozi wa Serikali, ujumbe wa Qatar na watendaji wengine  baada ya makabidhiano ya misaada ya kibinadamu kutoka Nchini Qatar


Kwa upande wake, Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Fahad Rashed Almarekhi, amesema msaada huo uliotolewa na nchi yake ni kielelezo cha kuthibitisha ukaribu na uhusiano mzuri uliopo baina ya Qatar na Tanzania na kwamba baada ya msaada huo watatuma timu ya wataalam kwenda kutambua mahitaji mengine ambayo hayakuguswa na msaada huo ili kutoa msaada mwingine ambao utakuwa ni suluhisho ya wananchi wa Hanang.
.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi.Queen Sendiga ameahidi kuhakikisha anasimamia vyema ugawaji wa misaada hiyo ili kuwafikia waathirika kama ilivyokusudiwa.