Back to top

SERIKALI YAANZA JUHUDI KUNUSURU MTO RUCHUGI

25 March 2024
Share

Serikali imeanza juhudi za kuunusuru mto Ruchugi katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, ambao ni tegemeo la wananachi kutokana na shughuli za kibinadamu kuuathiri na kusababisha kupungua kwa kina cha maji katika mto huo.

Wakizungumza wakati wa zoezi la kupanda miti zaidi ya elfu nne kandokando ya mto huo wananachi wanaoishi katika Vijiji jirani katika Kata ya msambara na Buhoro wilayani Kasulu wametaka watu wote wanaoendesha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi wachukuliwe hatua ili kulinda usalama wa maji yam to huo.

Afisa wa Mamlaka ya maji Bonde la Ziwa Tanganyika, Cornel Odemba, amesema kutokana na umuhimu wa mto huo serikali imetoa fedha zaidi ya shilingi milioni mia saba na ishirini ili kuurudisha mto huo katika hali yake kwa kupanda miti, kuweka alama na mabango yanayozuia watu kusogea umbali wa mita sitini kutoka mtoni.

Akiongoza zoezi la upandaji miti kandokando ya mto huo katika kata ya msambara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele, amewataka wananachi kuacha kufanya shughuli zinazoathiri mt huo kwa kuwa unategemewa na maelfu ya wananachi na kwamba serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha chanzo cha mto huo kinatunza.