Back to top

SERIKALI YASHAURIWA KUANZISHA KLINIKI YA FEDHA.

14 August 2024
Share

Serikali kupitia Wizara ya Fedha, kwa kushirikiana na Taasisi za kifedha ikiwemo Benki Kuu, Taasisi za Uwekezaji na Bima, zimeshauriwa kuanzisha kliniki ya elimu ya fedha kipindi cha mavuno, ili kuwafikia wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Bw. George Mbesigwe,  alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani humo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na  wanafunzi.

"Kipindi cha mavuno huku kwetu ndo kipindi ambacho wananchi wanakua na fedha, hivyo elimu hii ikitolewa wakati wa mavuno itasaidia wakulima kuhamasika kufungua akaunti benki, kufanya uwekezaji kupitia Taasisi za Uwekezaji au kukata Bima ya mazao kwakuwa zitakua zimefika katika eneo husika la mavuno" alisema Bw. Mbesigwe.

Naye Afisa Msimamizi Mkuu wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Salim Khalfan Kimaro, aliwashukuru wananchi wa Ruangwa kwa ushirikiano waliouonesha wakati wa semina kwa kuuliza maswali na kutoa ushauri ambao utazingatiwa awamu nyingine ya zoezi la utoaji elimu ya fedha.