Back to top

SILAA ATAKA MAKAMPUNI BINAFSI KUSAIDIA UPANGAJI NA UPIMAJI ARUSHA

07 April 2024
Share

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Slaaa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara yake kuhakikisha Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wamefika eneo la Olmoti linalotarajiwa kujengwa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa kisasa Jijini Arusha kufikia jumatatu asubuhi ya tarehe 8 Aprili 2024 ili waweze kuweka mpango wa Upangaji na upimaji wa eneo hilo.

Waziri Silaa amesema hayo wakati wa Hafla ya kumkabidhi Mkandarasi eneo la ujenzi wa Uwanja wa Kisasa wa Mpira wa Miguu unaotarajiwa kujengwa eneo  la Olmoti lililopo Jijini Arusha.

Aidha, Waziri Silaa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake kuhakikisha maeneo yote yanayozunguka uwanja huo wa michezo unaotarajiwa kujengwa ni lazima yawe yamepangwa na kupimwa ili kupusha makazi holela na migogoro ya ardhi hapo baadae.

Katika kuhakikisha jambo hilo linakamilika kwa wakati Waziri Silaa ametoa wito kwa Makampuni binafsi yanayojihusisha na kazi za upangaji na upimaji kushiriki katika kazi hiyo ya kupanga na kupima maeneo yote yanayozunguka uwanja huo wa mpira wa miguu.