Back to top

TADB YATAMBUA UBORA WA WANAFUNZI 13 SUA

08 October 2026
Share

‎Wanafunzi 13 wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) waliofanya vizuri katika masomo kwa mwaka 2026 wametunukiwa tuzo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuunga mkono wanafunzi wanaofanya vizuri katika taaluma zinazohusiana na sekta ya kilimo.
‎
‎Tuzo hizo zimetolewa leo, Oktoba 7, 2026, katika hafla iliyofanyika SUA, ambapo TADB imeshiriki katika kutambua na kuhamasisha wanafunzi hao kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao.
‎
‎Akizungumza kwa niaba ya TADB katika hafla hiyo, Afisa Rasilimali Watu Mkuu wa benki hiyo, Bi. Edna Nyatta, amesema TADB na SUA zina makubaliano ya ushirikiano (MoU) ambayo, pamoja na mambo mengine, yanawezesha benki hiyo kutambua na kuwaunga mkono wanafunzi wanaofanya vizuri katika taaluma zinazohusiana na sekta ya kilimo.


‎
‎Amesema TADB imeanzisha mpango wa “Learn with Us”, unaotoa fursa kwa vijana kupata uzoefu wa kujifunza kwa vitendo kupitia programu ya mafunzo kazini (Internship). Amesema takribani wanafunzi 10 kutoka SUA tayari wamepata nafasi za mafunzo kupitia mpango huo, huku sita kati yao wakifanikiwa kupata ajira za kudumu.
‎
‎TADB imeipongeza SUA kwa kuendelea kuzalisha wataalamu wanaohitajika katika sekta ya kilimo na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na chuo hicho katika kukuza vipaji na fursa kwa vijana.
‎
‎Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda, ameishukuru TADB kwa kushiriki katika utoaji wa tuzo hizo na kuiomba benki hiyo kutoa nafasi za mafunzo kazini kwa wanafunzi wote 13 waliotunukiwa tuzo.
‎
‎Amesema fursa hiyo itawasaidia wanafunzi hao kuunganisha elimu waliyoipata chuoni na uzoefu wa vitendo katika mazingira ya kazi, hatua itakayowaandaa zaidi kwa ajira na ujasiriamali katika sekta ya kilimo.