
Mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba umezinduliwa rasmi leo na Mkuu Mkoa wa Geita, Mhe. Alexander Mnyeti, kwa kupandikiza vifaranga vya samaki katika mojawapo ya vizimba vitakavyotumiwa na vijana 85 wanufaika wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika Wilaya ya Chato.
Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Maendeleo ya Vijana, na kuratibiwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) katika upatikanaji na usimamizi wa mitaji ya mikopo kwa wanufaika.

Akizungumza na vijana hao, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Alexander Mnyeti, amesema kuwa, “Vizimba ni utajiri ambao Serikali imewakabidhi mikononi mwenu,” huku akiwahimiza vijana hao kuwa wawajibikaji, kujituma na kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao. Aidha, amewataka kulinda na kutunza vitendea kazi na rasilimali walizokabidhiwa, hasa chakula cha samaki, pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na uadilifu na nidhamu katika usimamizi wa miradi hiyo. Amewasisitiza kutovumilia vitendo vya utovu wa nidhamu na kutokuwa waaminifu vinavyoweza kuhatarisha mafanikio na uendelevu wa miradi hiyo.
Programu hii inalenga kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mitaji na pembejeo za uzalishaji ili kuanzisha na kuendeleza miradi ya ufugaji a samaki kwa njia ya vizimba, kuongeza uzalishaji wa samaki na kujenga fursa endelevu za ajira na kipato.

Programu hiyo ilizinduliwa rasmi mwezi Machi 2026 Kanda ya Ziwa na imekuwa ikitekelezwa katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara. Kufika kwake katika Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, kunaashiria hatua nyingine muhimu katika kupanua wigo wa uwezeshaji wa vijana na kuimarisha shughuli za ufugaji wa samaki nchini.
Katika utekelezaji wa programu hii, TADB ina jukumu la kusimamia na kuratibu mikopo pamoja na kufuatilia matumizi na marejesho ya fedha hizo ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta matokeo tarajiwa ya mradi.
Ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kuwa endelevu kibiashara, TADB itaendelea kutekeleza majukumu yake ya utoaji wa mikopo kwa wakati Kuhakikisha upatikanaji wa mikopo na rasilimali za kifedha kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia mipango na ratiba zilizowekwa, Usimamizi na ufuatiliaji wa miradi, ushauri na elimu ya usimamizi wa fedha, usimamizi wa shughuli za uvunaji, Usimamizi wa marejesho ya mikopo kwa Kuhakikisha wanufaika wanarejesha mikopo kwa wakati na kwa mujibu wa masharti ya mikataba ili kuwezesha fedha hizo kuzunguka na kuwanufaisha vijana wengine kupitia programu hii.

