Back to top

TANZANIA NA CUBA ZASAINI MAKUBALIANO

15 September 2023
Share

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Cuba zimesaini Hati za Makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya elimu ya juu kwa kubadilishana wakufunzi na wanafunzi, kufundisha lugha ya kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana nchini Cuba pamoja na kutengeneza kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola.

Makubaliano hayo yamesainiwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba iliyofanyika Jijini Havana na kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia.

Mbali na Makubaliano ya elimu, makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam na Chuo Kikuu cha Havana ambapo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kiliwasilishwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. William Anangisye wakati Chuo Kikuu Cha Havana kiliwasilishwa na Prof. Miriam Garcia

Katika makubaliano hayo Tanzania na Cuba zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kupitia wahadhiri, wanafunzi, tafiti, sayansi, teknolojia, kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana na kutengeneza kamusi ya lugha ya Kiswahili na Kispaniola ili kusambaza matumizi ya lugha ya kiswahili nchini Cuba na nchi nyingine zinazozungumza lugha ya kihuspaniola.