Back to top

TAWIRI YAPONGEZWA KUWA NA MAABARA YA WADUDU.

09 June 2024
Share

Waziri  wa  Maliasili  na  Utalii  Mhe. Angellah  Kairuki (Mb), ameipongeza  Taasisi  ya  Utafiti  wa  Wanyamapori  Tanzania  (TAWIRI),  kwa kuthamini umuhimu  wa  wadudu  katika sekta ya uhifadhi  na kuanzisha maabara maalumu ya kuwahifadhi wadudu wote wanaopatikana  hapa nchini na nchi nyingine.

Waziri  Kairuki  ametoa pongezi hizo katika maonyesho  ya  Karibu  Kili Fair  2024 ambayo yamehitimishwa Jijini Arusha, ambapo pia ameelekeza taasisi hiyo kuona fursa za utalii katika swala zima la wadudu.

Aidha, ikiwa tafiti chache za wadudu zimefanyika  katika nchi  nyingi zinazoendelea huku kipaumbele  kikitolewa kwa wanyamapori wakubwa , TAWIRI  inajivunia 
kuwa na Maabara  hii ya wadudu ambayo ni kituo muhimu na sahihi kwa ajili ya kuhifadhi makundi mbalimbali ya wadudu yanayofanyiwa utafiti .

Akizungumza na Mwanahabari  wetu, Mtafiti wa Wadudu  kutoka TAWIRI Neema Kilimba amesema kupitia  maabara ya Wadudu, TAWIRI  kwa kushirikiana  na wadau wengine inakamilisha Kanzidata ya makundi mbalimbali ya wadudu wanaopatikana Tanzania na nchi nyingine. 

Vilevile  kupitia maabara hii, TAWIRI inaandaa orodha ya makundi mbalimbali ya wadudu na mtawanyiko wao nchini (atlas of insects) wakiwemo nyuki, mbawakawa wanaoviringisha vinyesi (dung beetles), wadudu wa maji baridi (aquatic insects of fresh water) na mbawakawa wanaoishi ardhini (carabidae - beetles)  

Mtafiti Kilimba  amebainisha, uwepo wa  kanzidata ya makundi mbalimbali ya wadudu utasaidia  kutambua aina mbalimbali za wadudu tulizonazo pamoja na makazi na mtawanyiko wao hivyo kuchochea uhifadhi wa bioanuwai hii muhimu,  kutoa elimu na msingi wa takwimu  kwa watafiti na wanafunzi mbalimbali. 

" uwepo maabara  ya  wadudu  umeamsha ari ya watafiti na wanafunzi kusoma na kufanya tafiti za wadudu ambao wanamchango mkubwa katika maisha ya binadamu, wanyama na mimea" amesema Mtafiti Kilimba

 Ameongeza Wadudu wanachangia uchavushaji  wa mimea  kwa zaidi ya asilimia  80%, uozeshaji na umeng'enyaji  wa taka hususani vinyesi na usafishaji wa mazingira(decomposition), uoteshaji wa mbegu mbalimbali, uongezaji mbolea kwenye udongo ( soil fertilization ), kuwezesha makazi ya wanyama wengine. Pia Wadudu ni chakula kwa wanyama wengine na sehemu muhimu kwenye mzunguko wa chakula (food chain)

Vilevile wadudu wanatumika kama viashiria vya afya ya mifumo ya kiikolojia. Wadudu wanachangia kwa asilimia kubwa kuongeza kipato kwa jamii kwa kuuza wadudu wenyewe kama chakula au bidhaa zitokanazo na wadudu.

TAWIRI  inawakaribisha wadau mbalimbali kujifunza kuhusu wadudu na ufugaji bora wa nyuki. Pia tunatoa elimu ya kisayansi (Scientific  talks) kuhusu wadudu na wanyamapori wengine kwa wadau wa utalii, wanafunzi na watafiti sambamba na kutoa ushauri (consultancy) ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii.