
Mamlaka za Mapato (TRA) Mikoa ya Ilala na Temeke jijini Dar es Salaam, zimepokea mashine mpya za kisasa, kwa ajili ya kukusanya maoni ya wateja, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha utoaji huduma ubora wa kwa wananchi.
Mashine hizo zitasaidia wananchi kutoa maoni kuhusu huduma wanazozipata. Kwamujibu wa Meneja wa TRA Mkoa wa Ilala, Eva Raphael, mashine hiyo inajiendesha yenyewe, ambapo mlipakodi akimaliza kupata huduma ina mpa nafasi ya kutoa maoni.
“Mashine hii inajiendesha yenyewe, Mlipakodi akimaliza mashine inampa nafasi ya kueleza huduma zetu zilikuwa kwa kiwango gani,amefurahia kwa kiwango cha juu,Kawaida,ama hakufurahia ama ni mbaya,"amesema Meneja huyo.
Ameongeza kuwa, taarifa zinazokusanywa zitatumika kuboresha utoaji huduma ili kuongeza ufanisi. Aidha, Eva amekumbusha walipa kodi juu ya wajibu wao wa kulipa Kodi ya Mapato ya awamu ya nne ambayo inalipwa mwezi Desemba.
“Niwakumbushe walipa kodi wetu kwamba mwezi wa Desemba ni kipindi cha malipo ya awamu ya nne ya Kodi ya Mapato,ni muhimu kutimiza wajibu huu kwa wakati,” amesema Meneja huyo.
Aidha,amewashukuru walipa kodi wote kwa ushirikiano wao wa muda mrefu, akisema mchango wao ndio unaowezesha TRA kufanikisha majukumu yake.
“Tunawashukuru sana kwa ushirikiano wenu. Mmeendelea kusimama nasi na kutuwezesha kufanya vizuri. Tunaomba tuendelee kushirikiana,” amesema Eva.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Temeke, Masau Malima, amesema kifaa hicho kimetua wakati muafaka katika kipindi ambacho Mamlaka inaweka nguvu kubwa kwenye ukusanyaji wa mapato kuelekea mwisho wa mwaka.
“Nielezee furaha yangu kuipata mashine hii katika ofisi ya Temeke,kwani imekuja wakati muafaka tukiwa na malengo makubwa na dhamira ya kuandika historia, lengo letu lipo pale pale kukusanya shilingi trilioni 4 kwa Desemba,” amesema
Amesema kuwa, lengo la kukusanya Sh. trilioni 4 kwa mwezi mmoja halijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka, lakini Temeke imejipanga kuvunja rekodi hiyo.
“Kwa mwezi mmoja tunalenga kukusanya Sh trilioni 4, jambo ambalo hatujawahi kufanya tangu Mamlaka ianze. Kama ilivyo kawaida yetu ya kuvunja rekodi, tumejipanga kuandika ukurasa mpya. Kwa hizi nyenzo tumeshaamka na tupo tayari kuanza safari kwa mbio za fasta sana,” amesema.
Kuhusu mashine alisema itasaidia kupokea maoni ya wateja kuhusu ubora wa huduma, jambo litakalowawezesha wataalamu wa TRA kubaini maeneo ya kuboresha, ili kuongeza ufanisi.
