Back to top

"TUCHUKUE HATUA KUPINGA VITENDO VYA UKATILI"- RAIS MWINYI

10 May 2025
Share

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, kuwalinda watoto na wanawake ili kulinda kizazi kijacho.

Dkt. Mwinyi ametoa rai hiyo leo katika uwanja wa Azimio Mtende wakati akizindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika mkoa wa Kusini Unguja ambapo ameongeza kuwa migogoro ni chanzo cha uvunjifu wa Amani katika jamii.

Dkt Mwinyi amesema jukumu la kukomesha ukatili na unyanyasaji wa kijinsia sio la mtu mmoja bali jamii nzima ikiwa ni pamoja na familia, viongozi wa dini na asasi mbalimbali huku akipongeza kampeni kwa kutoa elimu na utatuzi wa migogoro katika maeneo ya ukatili wa kijinsia, mirathi, na migogoro ya ardhi ambayo ndio chanzo cha uvunjivu wa amani.

Aidha Dkt. Mwinyi amesema kuwa serikali inaendelea kuimarisha mahakama na Taasisi zote zinazohusika na utoaji haki ili kuhakikisha upatikanaji wa haki na huduma za kisheria zinaimarika na kusogezwa karibu na wananchi kwa lengo la kushughulikia changamoto zao.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa Kisheria kwa upande wa Tanzania Bara Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini amesema jumla ya wananchi 2,774,495 wakiwemo wanawake 1,390,535 na wanaume 1,381,960 wamepatiwa huduma za Msaada wa Kisheria tangu kuzinduliwa kwa kampeni hiyo mwezi Machi 2023.

Mhe. Sagini ameongeza kuwa migogoro 5,704 imetatutliwa kati ya migogoro 23,399 ya muda mrefu iliyoibuka huku migogoro 18,987 ikiwa katika hatua mbalimbali za utatuzi na utekelezaji wa kampeni tayari umefikia Mikoa 25, halmashauri 180 na vijiji/mitaa 8702 ya Tanzania bara huku mkoa uliosalia wa Dar es Salaam ukitarajiwa kukamilika mwezi Juni 2025.

Kwa upande wao Chama cha Mawakili Zanzibar ZLS kimeahidi kuendeleza ushirikiano na serikali, Mahakama na wadau wengine wa sheria katika kuhakikisha dhamira ya serikali ya Kuifanya kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inakuwa endelevu kwani ndicho kiini cha utekelezaji wa utawala wa sheria na haki za binadamu nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Rais wa Chama Cha Mawakili Zanzibar (ZLS) Wakili Joseph Magazi ambaye amesema jitihada zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Mwinyi katika kuhakikisha kuwa huduma za Msaada wa kisheria zinamfikia kila mwananchi ni za kupongezwa.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, UWT Taifa Mary Pius Chatanda amesema Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia inayotekelezwa nchi nzima imekuwa msaada mkubwa kwa wanawake ambao wamekuwa wakisumbuliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mirathi.

Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe Ayoub Mohamed Mahmoud amesema utashi wa viongozi wa kitaifa wa kuhakikisha watanzania wanapata msaada wa kisheria umeifanya Tanzania kusifika Duniani kwa kujali watu wake.