Back to top

"TUTAHAKIKISHA TUNATOA HATI KUPITIA MRADI WA LTIP"- MHANDISI SANGA 

27 March 2024
Share

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema wizara yake itahakikisha inatoa Hatimiliki za Ardhi katika maeneo yote kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unatekelezwa.

Mhandisi Sanga amesema hayo wilayani Nzega wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu ya Serikali (PAC) ilipokwenda kukagua hatua iliyofikiwa na thamani ya fedha iliyotumika katika Utekelezaji mradi wa LTIP kwenye halmashauri ya Mji wa Nzega mkoani Tabora.

Kauli hiyo ya Mhandisi Sanga inafuatia baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kutaka utekelezaji mradi wa LTIP unaoendelea maeneo mbalimbali nchini kwenda sambamba na utoaji hati milki za ardhi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, kazi kubwa katika utekelezaji mradi huo wa LTIP ni kutambua, kupanga na kupima na hatua hizo zikishakamilika hati zote zinakuwa kwenye mtandao.

Akielezea zaidi kuhusu utekelezaji wa mradi wa LTIP katika halmashauri ya Mji wa Nzega mkoani Tabora, Mhandisi Sanga amesema kazi hiyo kwa sasa imetelekezwa kwa asilimia 55.

Ameongeza kuwa, hadi sasa vipande vya ardhi 18,655 vimetambuliwa, vipande 8,814 vimepangwa na viwanja 3,960 vimepimwa huku  Alama za Msingi za Upimaji 14 zikiwa  zimesimikwa ardhini.

Mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Mji wa Nzega imepewa lengo la kurasimisha vipande vya ardhi 20,000 ifikapo Juni 30, 2024 na kuongeza alama za msingi za upimaji 14.

Urasimishaji huo unatekelezwa katika mitaa 14 iliyopo kata 5 ambazo ni Nzega Mashariki, Nzega Magharibi, Nzega ndogo, Kitangiri pamoja na mtaa wa Uchama.

Kwa sasa utekelezaji wake unaendelea kwa zoezi la uhakiki wa taarifa za wananchi katika mtaa wa Nyasa, Msoma na Kitongo na upandaji wa mawe unaendelea katika mtaa wa uwanja wa ndege.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unatekelezwa kwa mkopo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milionin150 kutoka Benki ya Dunia kwa kupindi cha miaka 5 katika halmashauri 58 nchini. Mradi huo unalenga kuboresha utawala na usimamizi wa ardhi nchini pamoja na kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa wananchi.