
Mbunge wa Jimbo la Masasi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amekabidhi vifaa tiba katika Kituo cha Afya Mbonde, kilichopo Halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Dkt. Akwilapo amekabidhi vifaa hivyo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya katika Wilaya ya Masasi na maeneo jirani ya wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Dkt. Akwilapo amesema utoaji wa vifaa tiba ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha taasisi za huduma za jamii kama vile hospitali na shule zinakuwa na miundombinu na vifaa vinavyowawezesha wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.



Amesema, serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha sekta za afya na elimu zinaimarika ili wananchi waweze kupata huduma bora karibu na maeneo yao.
Ameongeza kuwa, kupatikana kwa vifaa tiba katika Kituo cha Afya Mbonde, ikiwemo mashine maalum ya kusaidia watoto waliozaliwa kabla ya muda, kutasaidia kuokoa maisha ya watoto hao.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mbonde, Dkt. Mohamed Abbas, amesema, vifaa vilivyopokelewa vitasaidia kuimarisha huduma mbalimbali ikiwemo huduma kwa watoto, chumba cha upasuaji pamoja na huduma za maabara.
