
Zaidi ya akina mama na watoto 150,740 waliokuwa na dharura ya huduma ya uzazi wamepata huduma ya usafiri wa haraka kupitia mfumo wa rufaa ngazi ya jamii (m-mama) ambapo hadi kufikia mwezi Mei, 2025 umeweza kuzuia vifo na kuokoa maisha ya wajawazito na watoto wachanga wapatao elfu 6,279.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe, amesema hayo kwenye kikao cha pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wenye lengo la kujadili namna ambavyo nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya mbali zimetumia mikakati mbalimbali ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ikiwemo ujenzi wa miundombinu, matumizi ya teknolojia, wahudumu ngazi ya jamii na mafunzo ya watumishi.
Katika kikao hicho, Mganga Mkuu wa Serikali ameelezea namna serikali ilivyowekeza katika kuboresha miundombinu ya afya hasa ngazi ya msingi ikiwemo majengo, vifaa na vifaa tiba na kuongeza vituo vinavyotoa huduma za Afya vyenye Huduma za dharura za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni ni 566 kufikia mwezi Machi, 2025.
"Pamoja na ujenzi wa miundombinu, bado tuliona kuna wajawazito ambao wanapopata dharura wanahitaji kusafirishwa kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine chenye huduma za ubingwa ili kupata huduma hizo na ndipo safari yetu ya M-Mama ilipoanza,"Amesema Dkt. Magembe
Amesema, "Safari yetu na m-mama imetupatia uzoefu ambao tuko tayari kushirikiana na jamii za Kimataifa ili kwa pamoja tuweze kupata suluhisho bunifu na za kiteknolojia kwa usafiri wa dharura ambao unaweza kuwa nafuu na endelevu katika maeneo ya pembezoni na yasiyofikika kirahisi.
Uzoefu wa Tanzania katika utoaji wa huduma za usafiri wa m-mama ni ubunifu unaoshirikisha sekta ya umma, binafsi na jamii katika kuboresha huduma za dharura kwa kuangalia mazingira na kutumia rasilimali zilizopo eneo husika.