Wizara ya Afya imesema tayari imetoa vipimo vya kuwawezesha wananchi kujipima wenyewe maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, vipatavyo 1,012,000, kwa mwaka 2023, ambapo 89% ya waliochukua vipimo hivyo waliweza kurudisha majibu, baada ya kujipima.
.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe.Ummya Mwalimu, leo Disemba 01, 2023, katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Morogoro, ambapo amebainisha kuwa wataendelea kutoa vitendanishi hivyo, ili kuwawezesha wananchi kupata wepesi pindi wanapohitaji kujua hali zao za kiafya hasa hali ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
.
Aidha, Waziri Ummy amesema wameamua kujumuisha mapambano dhidi ya UKIMWI pamoja na masula ya magonjwa ya ngono na homa ya ini, baada ya takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), kuonyesha kwamba kuna kushabihiana katika njia za maambukizi, udhibiti na tiba ya magonjwa hayo, na kwamba mnamo Novemba 24, 2023, uliokuwa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI yaani National AIDS Control Program (NACP), umeongezewa majukumu ya kuratibu na kusimamia huduma za magonjwa ya kuambukizwa kwa njia ya ngono na homa ya ini.
.
Hivyo, mpango huo kwa sasa, unatambulika rasmi kama National AIDS, STIs and Hepatitis Control Program (NASHCoP)” alisema Waziri Ummy.