Back to top

WAFUGAJI WATAKIWA KUTENGA MAENEO YA MALISHO KWA AJILI YA KIANGAZI.

22 April 2023
Share

Wafugaji kote nchini katika msimu huu wa mvua, wametakiwa kutenga baadhi ya maeneo ya malisho na kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi wakati wa kiangazi, ili kuepuka migogoro baina yao na wakulima.

Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia wizi wa Mifugo nchini ACP Simon Pasua, ameyasema hayo leo wilayani Monduli, wakati alipokutana na viongozi wa wafugaji pamoja na wakulima, kwa lengo la kupanga mikakati ya pamoja ya kuepusha migogoro, ambayo imekuwa ikijitokeza wakati wa kiangazi.

Kamanda Pasua amebainisha kuwa wakati wa kiangazi kuna kuwa na ukame, hivyo kupelekea changamoto za kukosekana sehemu za malisho hali ambayo inasababisha baadhi ya wafugaji kupeleka mifugo sehemu ambazo sio rasmi.

Lakini pia amewataka kupanga matumizi bora ya ardhi, pamoja na kuacha kupelekea mifugo maeneo ya vyanzo vya maji, ili kuepuka migogoro ambayo inaweza kujitokeza lakini pia kukauka kwa vyanzo hivyo.

Mwisho ametoa wito kwa wafugaji pamoja na wakulima, kuwa na vikao vya maridhiano na kutumia vikundi vya ulinzi shirikishi pindi migogoro inapotokea kuepuka uvunjifu wa amani.