Back to top

Wafungwa sitini na tatu wanufaika na mpango wa Parole Arusha.

09 May 2018
Share

Jumla ya wafungwa sitini na tatu waliokua wakitumikia vifungo vya aina mbalimbali katika magereza za mkoa wa Arusha wamenufaika na mpango wa Parole unaotoa nafasi kwa mfungwa kutumikia kifungo cha nje baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na bodi ya Parole ya taifa kwa mujibu wa sheria.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa taarifa ya katibu wa bodi ya Parole ya mkoa wa Arusha kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la Magereza Hamisi Nkubasi aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa bodi ya saba ya Parole ya mkoa ambaye pia anazitaja baadhi ya changamoto zinazokabili utekelezaji wa mpango huo kuwa ni pamoja na bajeti finyu ya kufuatilia taarifa za wafungwa husika.

Mwalimu mstaafu David Marandu ndiye Mwenyekiti wa bodi hiyo mpya anatoa wito kwa wajumbe wenzake kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria ili kufikia lengo la serikali la kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani huku katibu tawala wa mkoa wa arusha  richard gwitega akisisitiza umuhimu wa jamii kutoa ushirikiano.

Mpango wa Parole ulianzishwa rasmi hapa nchini baada ya kupitishwa kwa sheria ya bodi ya Parole no 25 ya mwaka 1994 na sheria yake kuanza kutumika mwaka 1999 kwa lengo la  kuwasaidia wafungwa wanaokidhi vigezo  kuwa karibu na familia wakiwa wanaendelea kutumikia adhabu,kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na kuipunguzia serikali gharama za uendeshaji.