Back to top

WAKAZI ELFU ISHIRINI KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI NEWALA

06 April 2023
Share

Wananchi zaidi ya Elfu 20, katika Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara wanatarajiwa kunufaika na mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2, uliyojengwa katika Kijiji cha Mnaida kata ya Lidumbe.

Mradi huo unatarajiwa kuondoa changamoto ya maji iliyodumu kwa miaka thelathini katika vijiji kumi na tatu vya kata ya lidumbe wilaya ya newala.

Wakizungumza mara baada ya mwenge wa uhuru  kuweka jiwe  la msingi  katika mradi wa maji wa mnaida baadhi ya wanachi   kijiji  hicho wamesema kupatikana kwa maji safi na salama kutabadilisha maisha yao.

Wamesema walikuwa wanalazimika kutembea Kilomita 9 kutafuta maji kwenye mabonde hasa kipindi cha kiangazi hali iliyokuwa ikipelekea kukosekana kwa maendeleo katika vijiji hivyo.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Newala Sadick Nsajigwa, amesema mradi huo umejengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 2 na utahudumia Vijiji kumi na tatu kutoka kata ya Lidumbe.

Amesema kupatikana kwa maji  katika vijiji hivyo kutachochea maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na elimu ambapo  wanafunzi walikuwa wakishindwa kuhudhuria masomo ipasavyo kutokana na changamoto ya maji katika vijiji hivyo.