Back to top

WALIMU WANAOTOA ADHABU ZA KIKATILI SHULENI KUKIONA

02 February 2023
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, amesema serikali haitafumbia macho suala la adhabu shuleni linalofanywa na baadhi ya walimu kwa kukiuka sheria na taratibu na kusababisha madhara kwa jamii, na tayari serikali imeshachukua hatua kwa wahusika.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo bungeni Dodoma, ambapo amebainisha kuwa adhabu itazingatia ukubwa wa kosa, jinsia na afya ya mtoto na isizidi viboko 4 kwa wakati mmoja, mwanafunzi wa kike atapewa adhabu mkononi na mwalimu wakike, isipokuwa kama shule hiyo haina mwalimu wa kike.

Waziri Mkuu amesema adhabu ya viboko itakapotolewa iorodheshwe katika kitabu kilicho tengwa kwa ajili ya hiyo ikiwa ni pamoja na jina la mwanafunzi aliyepewa adhabu, kosa alilotenda, idadi ya viboko, na jina la mwalimu aliyetoa adhabu hiyo.

Pia amefafanua kuwa mwalimu mkuu lazima atie saini katika kitabu kila mahala baada ya adhabu hiyo inapotolewa, na pia mwanafunzi akikataa adhabu ya viboko atasimamishwa shule.

Aidha hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa Mwalimu yeyote ambaye atakiuka utaratibu wa adhabu ya viboko, na hatua kali zitachukuliwa hata kwa walimu wakuu ama walimu wa shule wanaokiuka utaratibu uliowekwa.