
Miili ya watu 11 kati ya watu 12 waliofariki katika ajali ya basi la abiria mali ya kampuni ya Freste R yenye namba za usajili T415 DPP, ikitokea Bukoba kwenda Dar es Salaam na lori aina ya Texas, likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma imepokelewa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya utambuzi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Daktari Kessy Ngalawa, amesema hayo hospitalini hapo na kubainisha miongoni mwa miili hiyo, wamo wanawake watatu, wanaume saba na mwili mmoja wa mtoto wa kike anaekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka minne na mitano.

Dkt.Ngalawa amesema mpaka sasa ni miili ya watu wawili tu, imetambuliwa kwa majina hadi sasa na utaratibu zaidi unaendelea ili kuwatambua marehemu wote waliopokewa katika hospitali hiyo.
Mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye tayari mwili wake umeshatambuliwa Hamis Issa, alisema marehemu ndugu yake alikua ni askari na aliongozana na askari mwenzie kumfuata mtuhumiwa ili kumpeleka Jijini Dar es Salaam, ambapo askari hao wawili walipanda basi hilo la kurejea Dar es Salaam mpaka walipofikwa na umauti.
Ajali hiyo imetokea usiku wa saa tisa, kuamkia leo katika kijiji cha Silwa, Kata ya Pandambili Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma na kusababisha vifo vya watu Kumi na wawili pamoja na majeruhi sitini na watatu.

