Back to top

Wananchi wajitokeza kujenga vyumba vya madarasa kwa nguvu zao Mbeya

11 January 2020
Share

Mamia ya wakazi wa mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, wamejitokeza kushiriki kazi ya ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa kwa kutumia nguvu zao katika shule ya sekondari Usongwe ili kuwezesha wanafunzi zaidi ya 400 ambao wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu kuanza masomo.

Shule ya sekondari ya Usongwe inatakiwa kupokea wanafunzi 900 wa kidato cha kwanza mwaka huu, lakini kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, ni wanafunzi 500 pekee ndio ambao wameanza masomo mpaka hivi sasa, hali ambayo imewasukuma wananchi kujitokeza kwa wingi kujenga vyumba tisa vya madarasa vinavyohitajika kwa kutumia nguvu zao ili kuruhusu wanafunzi 400 waliobaki kuanza masomo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mbalizi, Paulo Mwampamba amesema utamaduni wa wananchi kujitolea nguvu zao kufanya shughuli za maendeleo, ni mzuri kwa vile unaokoa fedha na kuondoa ubaguzi wa kipato miongoni mwao

Wakati wananchi hao wakiendelea na kazi, likawasili gari likiwa limesheheni mifuko 100 ya saruji ambayo imetolewa na mbunge wa Mbeya vijijini Mhe.Oran Manase Njeza, ambaye amewataka wananchi kuendelea na moyo huo wa kujitolea ili shule hiyo ikamilike na wanafunzi waanze masomo mara moja.