Back to top

WANANCHI WAPATIWA MSAADA WA KISHERIA TABATA DSM

07 July 2024
Share

 Wataalam wa Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Shirika la Citizens Foundation, wametoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa mamia ya Wananchi wa Wilaya ya Ilala, ikiwa ni mwendelezo wa dhamira ya dhati ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,  kuhakikisha Wananchi wote wanafikiwa na huduma hiyo inayotolewa kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign.

Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hiyo iliyofanyika katika viwanja vya shule ya Tabata Wilaya ya Ilala Jijini Dar- es Salaam,  Wakili wa Serikali Kandibu Nasua na Menegati John,  wamesema wanaendelea kazi ya kutoa huduma hiyo ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro na changamoto mbalimbali zinazohusiana sheria pamoja na kutoa elimu kuhusu masuala ya sheria.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Citizens Foundation Bi. Lilian Wassira, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuwajali na kuwapenda Wananchi wake na ndio maana ameamua kuwapelekea huduma hiyo hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kupata utetezi wa kisheria sambamba na wale wenye changamoto ambazo hazijatatuliwa kwa sababu mbalimbali.